/, Educative, Swahili, Women's Health, Youth/Kitanzi njia rahisi na nafuu kwa uzazi wa mpango

Kitanzi njia rahisi na nafuu kwa uzazi wa mpango

2020-09-16T17:52:47+03:00 September 15th, 2020|Blog, Educative, Swahili, Women's Health, Youth|

Panga uzazi wa muda mrefu na Kitanzi.

Kitanzi ni nini? Je kitanzi kinakaa wapi katika mwili wa mwanamke? Naweza kupata wapi? Je ninamuhitaji daktari kwa ajili ya kuwekewa kitanzi? Je kinafanya kazi kwa muda gani?

Utangulizi.

Kitanzi ni kifaa kidogo kilichotengenezwa kwa plastiki na chenye umbo la T ambacho huwekwa ndani ya tumbo la uzazi(uterasi) ili kuzuia ujauzito. Ni njia ya uzazi wa mpango ya muda mrefu na moja ya njia zenye ufanisi mkubwa katika kuzuia ujauzito.

Vitanzi vinapatikana hospitali, katika vituo vya afya au kliniki na kwa gharama nafuu. Kitanzi kinapaswa kuwekwa na daktari au mhudumu wa afya kwa umakini zaidi.

Kitanzi huzuia ujauzito kwa muda wa miaka 5 hadi 10 kutegemeana na aina ya kitanzi.

Aina za Vitanzi

  • Kitanzi chenye kichocheo (homoni)

Hiki ni kitanzi ambacho kina homoni ya projestini ambayo ni sawa na homoni ya projesterone iliyopo katika miili yetu na hutolewa kwa kiasi kidogo baada ya miaka 5-10. Kitanzi hiki huzuia ujauzito kwa kuweka manii(shawaha) mbali na mayai (ovari). Kitanzi chenye homoni huzuia ujauzito kwa njia mbili:

  1. Hutengeneza ute ambao hufanya ukuta wa mlango wa kizazi kuwa mnene hivyo kuzuia shahawa kulifikia yai (ovari)
  2. Huzuia mayai kutoka kwenye mfuko wake hivyo hakuna ututubishaji wa yai.
  • Kitanzi kisicho na kichocheo (homoni)

Hiki ni kitanzi ambacho hakina homoni hivyo hutumia madini ya shaba kuzuia ujauzito. Madini ya shaba hubadilisha mazingira ya tumbo la uzazi hivyo shawaha kushindwa kulifikia yai na kufanya urutubishaji.

Dhana potofu kuhusu Kitanzi (Njia ya uzazi wa mpango ya muda mrefu)

  1. Kitanzi kinaweza kuumiza uume
  2. Kitanzi husababisha utasa/ugumba wa muda mrefu
  3. Kitanzi kinaweza kusafiri kutoka kwenye mfuko wa uzazi kupitia utumbo na kufika kwenye moyo.
  4. Kitanzi kinaweza kusababisha maumivu makali ya tumbo na mgongo.

Hakuna ukweli kuhusu dhana hizi isipokuwa dhana namba nne(4) inaweza kutokea kwa baadhi ya wanawake na hupotea baada ya muda fulani.

“Je kitanzi kinaweza kumuumiza mpenzi wangu?”

Hapana: Inawezekana umesikia kwamba nyuzi za vitanzi zinaweza kuwasumbua wanaume wakati wa kufanya mapenzi, lakini walio wengi hawawezi kuhisi nyuzi hizo. Ikiwa mwenzi wako anazihizi na zinamletea usumbufu wasiliana na mtoa huduma wako wa afya ili aweze kuzipunguza. Pia vyuzi hizo huweza kuwa laini baada ya muda fulani.

“Itakuwaje iwapo napatwa maumivu makali ya tumbo kipindi cha hedhi?”

Kawaida hiyo haitokei sana. Jaribu kwa miezi michache, na endapo unapatwa na maumivu ya tumbo tumia dawa za kutuliza maumivu (ibuprofen), baada ya siku za kwanza za hedhi maumivu yote yatatoweka. Ikiwa unapenda kutumia njia ya kitanzi lakini maudhi madogomadogo hayatoweki baada ya muda fulani, unaweza kujaribu njia nyingine kama kipandikizi.

“Je nifanyaje ikiwa nataka kupata ujauzito?”

Ikiwa uko tayari kupata ujauzito, wasiliana na mtoa huduma wako wa afya ili aweze kukitoa kitanzi. Mara tu baada ya kitanzi kutolewa mwili wako utarudi katika hali ya kawaida na utaweza kupata ujauzito.

“Ninahitaji kukitoa kitanzi. Je! Ninaweza kukitoa mwenyewe?”

Unaweza kuwa umesikia habari mitandaoni kuhusu watu kujitoa vitanzi vyao wenyewe. Hatushauri kufanya hivyo, siyo salama. Ikiwa unataka kutoa kitanzi, nenda kwa mtoa huduma wako wa afya aweze kukitoa. Hii itakupa pia nafasi ya kuzungumza juu ya njia nyingine za uzazi wa mpango au jinsi ya kupata ujauzito na vitu unavyopaswa kufanya ili kujiandaa kwa ujauzito mzuri.

“Je! Ninaweza kutumia kitanzi ikiwa ninaishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU)?”

Wanawake wanaoishi na VVU wanaweza kutumia kitanzi na kikawekwa kwa usalama ikiwa wana udhaifu mdogo kiafya au hawana ugonjwa wowote uliothibitishwa kidaktari hata kama wako kwenye tiba ya kurefusha maisha au la.